Mary Matia, mfanyabiashara msichana mwenye umri wa miaka 23, anaweza kuwa aliingiwa na huruma wakati aliposhuhudia vifaranga 6,400 wa kuku aliowanunua Kenya wakichomwa moto, lakini kilio kikuu kilikuwa ni jinsi ya kurudisha fedha alizotumia kuwanunua.
Matia alikuwa akijaribu kuingiza vifaranga hivyo nchini kwa njia za panya na alinaswa eneo la Namanga mpakani mwa Tanzania na Kenya.
Kosa lake kubwa lilikuwa ni kukiuka tangazo la Serikali lililotolewa miaka kumi iliyopita la kuzuia kuingiza vifaranga na mayai kutoka nje ya nchi na kuvisambaza nchini.
Juhudi za Matia kubembeleza maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ili avirejeshe Kenya kwa ajili ya kurejesha japo sehemu ya fedha zake, zilishindikana na badala yake akawa mmoja wa mashuhuda wakati vifaranga hao wakichomwa moto.
“Nimewaomba tuvirejeshe Nairobi niliponunua, wamegoma,” alisema Matia baada ya vifaranga hao kuchomwa moto eneo la Namanga. “Mimi nilikuwa sijui kama ni makosa kununua vifaranga Kenya.”
Alisema amekuwa akijihusisha na biashara ya kuku na alinunua vifaranga hivyo kwa Sh 12.5 milioni ili kuvikuza na baadaye kuuza.
“Nimepata hasara kubwa. Nilikuwa nimekopa fedha sijui nitarudisha vipi,” alisema.
Mfanyabiashara huyo alisema juzi ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupitisha vifaranga hivyo, lakini anamiliki mabanda ya kuuza kuku katika eneo la Mianzini katika jiji la Arusha.
Kazi ya kuchoma moto vifaranga hivyo ilifanyika jana katika eneo maalumu la kuchoma bidhaa zisizo na ubora lililopo Namanga na liliendeshwa na maofisa wa TFDA, Wizara ya Mifugo, Mamlaka ya Mapato (TRA) na vyombo vya usalama.
“Tumevichoma moto, ili visisambazwe tena hapa nchini kwa kuwa hatujui usalama wake, hasa kutokana na kuwepo taarifa za ugonjwa wa mafua ya ndege nchi jirani,” alisema ofisa mfawidhi wa Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa ya Mifugo Kanda ya Kaskazini, Obedi Nyasebwa.
Nyasebwa alisema wameteketeza vifaranga hivyo kwa kuzingatia Sheria ya Magonjwa ya Wanyama namba 17 ya mwaka 2003 na tangazo la mwaka 2007 la kupiga marufuku kuingizwa nchini vifaranga vya kuku na mayai.
Meneja msaidizi wa TRA wa Namanga, Edwin Iwato alisema gari la mfanyabiashara huyo pia litaendelea kushikiliwa kwa kosa la kuingiza nchini bidhaa ambao zimepigwa marufuku.
No comments:
Post a Comment