Spika wa Bunge la Ethiopia amejiuzulu kwa kile kinachotajwa kuwa ni kuonesha malalamiko yake dhidi ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya nchi hiyo dhidi ya watu wa kabila la Oromo
Abadula Gemeda mwenyewe hakuweka wazi sababu ya kujiuzulu kwake na amesema atatangaza sababu hiyo baada ya Bunge kupasisha barua ya kujiuzu.
Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya Pembe ya Afrika wanasema Abadula ambaye anatoka kabila la Oromo, amechukua uamuzi wa kujizulu akipinga jinsi serikali ya Addis Ababa ilivyokabiliana na machafuko yaliyolikumba eneo la Oromiya mwaka 2015 na 2016.
Machafuko hayo yaliifanya serikali ya Ethiopia kutangaza hali ya hatari kote nchini humo kwa kipindi cha miezi 9.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Kamisheni ya Haki za Binaadamu nchini Ethiopia, maandamano ya wananchi ya mwaka jana yalipelekea kuuawa watu wasiopungua 669 na kwamba 462 kati yao walikuwa wakazi wa eneo la Oromia.
Wakati huo huo Shirika la Msamaha Duniani (Amnesty International) limetangaza kuwa idadi ya waliouawa katika maandamano hayo ya mwaka jana ni watu 800.
Vilevile Umoja wa Mataifa anaitaka serikali ya Addis Ababa kuwaachia huru wapinzani zaidi ya elfu 26 waliotiwa mbaroni katika maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo.
Wapinzani ambao wengi ni wa kabila la Oromo wanataka kufanyika marekebisho ya kisiasa na kijamii ikiwa ni pamoja na kukomeshwa ukiukaji wa haki za binadamu, mauaji dhidi ya raia wa kawaida, kamatakamata na ukandamizaji wa kisiasa dhidi ya makundi ya upinzani.
No comments:
Post a Comment