Tambo za wiki nzima, utani wa hapa na pale, Yanga na Simba zimetoshana nguvu baada kutoka sare ya bao 1-1 katika mchezo mkali uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 57 kupitia kwa Shiza Kichuya aliyemalizia pasi ya Erasto Nyoni ambaye naye aliuwahi mpira uliopanguliwa na kipa wa Yanga, Youth Rostand wakati akiokoa krosi ya Emmanuel Okwi.
Dakika tatu baadae, Yanga ilisawazisha bao hilo kupitia kwa Obrey Chirwa aliyemalizia kwa shuti la kawaida pasi ya Geofrey Mwashiuya.
Timu zote zilianza mpira kwa kasi kipindi cha kwanza huku Simba ikionekana kumiliki mpira zaidi, lakini ilikuwa haiko vizuri katika umaliziaji wakati Yanga ilikuwa ikifanya mashambulizi ya kustukiza kupitia kwa Chirwa na Ajib.
Wachezaji wanaotajwa sana kwa sasa na mashabiki wa soka hapa nchini kutokana na aksi yaop ya ufungaji, Ajib wa Yanga na Emmanuel Okwi wa Simba walidhibitiwa vilivyo na mabeki wa timu zote mbili hivyo kushindwa kupachika bao katika mchezo huo.
Kipindi cha pili Yanga walionekana kuja na mbinu mpya na kufanya mashambulizi kadhaa golini kwa Simba, lakini safu ya ulinzi iliyoongozwa na Method Mwanjali ilikuwa makini.
Hata hivyo kipindi cha pili kulikuwa na rafu za mara kwa mara kwa timu hizo na kupelekea Ajib na Juma Abdul kupewa kadi ya njano huku kwa upande wa Simba aliyeonyesha kadi ya njano ni Kichuya baada ya kuvuka hadi kwa mashabiki kushangilia bao lake alilofunga.
Katika mchezo huo Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Laudit Mavugo,James Kotei na Mzamiru Yassin na kuwaingiza John Bocco, Jonas Mkude na Said Ndemla wakati Yanga iliwatoa Geofrey Mwashiuya na Raphael Daud na kuwaingiza Emmanuel Martin na Pato Ngonyani.
Kutokana na matokeo hayo, Simba imerejea kileleni kwa kufikisha pointi 16 sawa na Yanga na Azam, lakini ikiongoza kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
No comments:
Post a Comment