Serikali ya Austria imeanza kutekeleza rasmi marufuku ya wanawake Waislamu kuvaa hijabu inayofunika uso wote maarufu kama burqa au niqabu katika maeneo yote ya umma nchini humo.
Carla Amina Bhagajati, afisa wa Jumuiya ya Waislamu Austria amelaani marufuku hiyo na kusema kuwa hatua hiyo ni ya kinafiki ambayo itapelekea jamii ya nchi hiyo ipoteze thamani zake.
Mwanaharakati huyo amenukuliwa na kanali ya Press TV ya Iran akisema kuwa, wanawake wachache wa Kiislamu wanaovaa niqabu anaowafahamu katika mji wa Vienna kwa sasa wanaonekana kama wahalifu, na baadhi yao wamelazimika kubakia majumbani mwao.
Watakaokiuka marufuku hii watapigwa faini ya Euro 150, huku polisi ikipewa idhini ya kutumia nguvu kwa wale watakaokataa kuonyesha nyuso zao.
Nchi kadhaa za magharibi kama vile Bulgaria, Canada, Ubelgiji na Ufaransa zimepiga marufuku vazi hilo la staha.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Ushauri kwa Waislamu Austria, kati ya watu milioni tisa nchini humo, takribani laki 6 ni Waislamu.
Hii ni katika hali ambayo, uchunguzi wa maoni uliofanywa mwaka jana na Idara ya Takwimu nchini Australia ulionyesha kwamba, katika kipindi cha kati ya miaka 1991 na 2016, kasi ya watu kuingia katika dini ya Uislamu imeongezeka kwa asilimia 160.
No comments:
Post a Comment