Idara ya Huduma za Kijamii nchini Bangladesh imesema watoto karibu 14 elfu wa Rohingya wamekuwa mayatima baada ya kupoteza wazazi wao katika mauaji yanayofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii hiyo nchini Myanmar.
Pritam Kumar Chowdhury, Naibu Mkurugenzi wa idara hiyo ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, watoto wadogo wamayatima wapatao 13,751 wamekusanyika katika kambi za wakimbizi nchini humo, baadhi wamepoteza wazazi wote wawili na wengine mmoja.
Amesema baadhi ya watoto hao wamekimbilia Bangladesh bila mtu wa familia au hata msimamizi.
Wakati huo huo, Waislamu 12 wa jamii ya Rohingya wakiwemo watoto wadogo sita wamefariki dunia leo Jumatatu katika Mto Naf katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh baada ya boti yao kuzama, wakikimbilia usalama wao nchini Bangladesh.
Sheikh Ashrafuzzaman, afisa mmoja wa polisi amesema boti hiyo iliyokuwa imebeba watu 65 imezama karibu na eneo la Bengal, karibu na kijiji cha uvuvi cha Shah Porir Dwip cha Bangladesh.
Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitahadharisha kuwa, hali ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya wapatao laki nane huko Bangladesh inatia wasi wasi mkubwa na kwamba wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.
Mamia ya maelfu ya Waislamu wa Rohingya wamelazimika kukimbilia Bangladesh kutokana na mauaji na ukandamizaji wa jeshi la nchi hiyo wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya jamii hiyo ya waliowachache katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment