Polisi nchini Kenya jana imetumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa upinzani zaidi ya elfu moja waliokuwa wakiandamana katika mji mkuu Nairobi wakitaka kuweko mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Aidha polisi ya Kenya ilitumia pia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji wa upinzani katika mji wa Kisumu ambao ni ngome ya kinara wa upinzani Raila Odinga.
Wafuasi hao wa upinzani mjini Kisumu walikataa kutawanyika licha ya kuhutuniwa na Anyang Nyong'o Gavana wa kaunti hiyo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga jana alitangaza kuwa hatogombea katika uchaguzi wa marudio wa rais ulioamriwa kuitishwa tena na Mahakama ya Juu ya nchi hiyo ambao umepangwa kufanyika tarehe 26 Oktoba akisema kwamba, uchaguzi huo hautokuwa huru na wa haki.
Raila Odinga amesisitiza kuwa, muungano wa upinzani wa NASA umefikia hitimisho kwamba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC haina nia ya kuhakikisha ukiukaji wa taratibu na sheria za uchaguzi uliofanywa na tume hiyo katika uchaguzi uliopita hautokei tena.
Wakati huo huo, Rais Uhuru Kenyatta amesisitiza kuwa uchaguzi huo wa marudio utafanyika kama ilivyopangwa licha ya mshindani wake kujitoa.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, uamuzi wa mgombea wa chama kikuu cha upinzani wa kujiondoa katika uchaguzi wa marudio wa rais zikiwa zimebakia siku 16 tu kabla ya zoezi hilo kufanyika, unaweza kuwa na taathira hasi za kisiasa nchini Kenya na hata kusababisha ghasia na machafuko.
No comments:
Post a Comment