Tuesday, September 19, 2017

19 September 2017,NIGERIA: Watu wapatao 44 wamepoteza maisha kutokana na mlipuko wa Kipindupindu na milioni 3.7 wako hatarini kuambukizwa

Watu wapatao 44 wamefariki kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu ,milioni 3.7 wako hatarini katika Jimbo la Borno, kaskazini-mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA, jitihada za kuzuia na kukabiliana na mlipuko huo zimeimarishwa ili kushughulikia mahitaji ya haraka ya watu wapatao milioni 3.7 ambao wako hatarini kuambukizwa.

Licha ya juhudi kubwa za kuboresha usafi wa mazingira katika makambi na kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa mazoea ya usafi, matukio ya kwanza ya kipindupindu yalitokea katika Jimbo la Borno tarehe 16 Agosti.

Hadi sasa, watu wapatao 44 tayari wamepoteza maisha kutokana na mlipuko huo, kati ya visa 2,300 vilivyothibitishwa.

Naye Mratibu wa OCHA Nigeria Lundberg amesema wanahitaji mbinu sahihi ya kukabiliana  na mlipuko huo ili kuokoa maisha ya mamilioni ya watu walioko kwenye maeneo yenye migogoro.

Ameongeza kua mashirika ya kibinadamu yamekuwa yakifanya kazi kwa ukaribu  sana na wizara ya afya jimboni Borno ili kuzuia kuzuka kwa kipindupindu katika maeneo mengi.

Jimbo la Borno ni ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limekuwa likitekeleza hujuma za kigaidi kaskazini mwa Nigeria na kupelekea kuporomoka huduma za afya eneo hilo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mashambulio ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram yaliyoanzia kaskazini mwa Nigeria na kusambaa hadi ndani ya ardhi za nchi jirani za Cameroon, Chad na Niger yameshaua zaidi ya watu 20,000 katika eneo lote la Bonde la Ziwa Chad linalojumuisha nchi hizo nne, mbali na kuwafanya watu wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi.

No comments: