Nigeria imelaani maangamizi yanayofanyika nchini Myanmar dhidi ya jamii ya Waislamu wa Rohingya na kuutaka Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake na kusitisha operesheni za kijeshi za kuwahamisha kwa mabavu Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Nigeria aimesema kuwa: Abuja inalaani vikali maafa ya binadamu ambayo yametajwa na Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kuwa ni maangamizi ya kizazi cha jamii ya Rohingya.
Taarifa hiyo imesema kuwa, yanayofanyika Myanmar yanakumbusha yaliyotokea Rwanda na Bosnia Herzegovina ambako kulifanyika mauaji ya kimbari katika miaka ya 1994 na 1995.
Serikali ya Nigeria imewataka wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusimamisha umwagaji wa damu huko Myanmar na kufanya jitihada za kukomesha machafuko na kutayarisha mazingira mazuri na salama kwa ajili ya kuwarejesha makwao mamia ya maelfu ya wakimbizi wa Rohingya.
Umoja wa Mataifa unasema kuwa zaidi ya Waislamu laki tatu na 70 elfu wa jamii ya Rohingya wamelazimishwa kukimbia miji na makazi yao tangu tarehe 25 mwezi uliopita wa Agosti.
Maelfu ya Waislamu wa jamii ya Rohingya pia wameuawa katika mashambulizi yanayoendelea kufanywa na mabudha wenye misimamo ya kuchupa mipaka wakisaidiwa na jeshi la Myanmar.
No comments:
Post a Comment