Tuesday, August 1, 2017

1 August 2017, Kombe haliendi Simba walaYanga-Mwigulu

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ambaye ni mlezi wa timu ya Singida United amefunguka na kusema msimu huu kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara halitakwenda Simba wala Yanga na kusema kombe litakwenda timu za mikoani.

Mwigulu Nchemba amesema hayo jana baada ya timu yake Singida United kucheza na timu ya Lipuli FC ya Iringa, mchezo ambao uliwafanya Lipuli FC kutamba kwa kuipiga Singida United bao moja kwa sifuli.

"Tutaweka jitihadi kila zinazowezekana ili tuunge mkono maono ya Rais Magufuli, Rais ameondoa serikali Dar es Saalaam na kuileta Dodoma na sisi tutaliondoa kombe Dar es Salaam na kulileta mikoani ili ile hali ya kila kitu kuzoeleka Dar es Salaam ifike mwisho, timu zipo nyingi na hizi timu ambazo ziko karibu na serikali Dodoma zinaweza kupata ubingwa" alisema Mwigulu Nchemba

Mbali na hilo Mlezi wa timu ya Lipuli FC ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amesema kuwa jambo hilo linawezekana na kusema kwa kuwa haijaandikwa katika vitabu vya dini kuwa lazima kombe libaki jijini Dar es Salaam basi msimu huu kombe litaondoka jijini humo na kwenda mkoani kutokana na timu zao zilivyojipanga kuleta ushindani wa kweli.

"Hakuna mahali kwenye Biblia au Quran Tukufu pameandikwa kwamba Kombe la mashindano ya mpira wa miguu lazima libaki Dar es Salaam na kwa kuwa haikuandikwa wala hakuna kanuni hiyo na sheria basi lazima tujipange kuliondoa" alisema Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Lipuli FC kutoka mkoani Iringa, Singida United kutoka mkoani Singida na Njombe Mji kutoka Njombe ni timu ambazo zimepanda Ligi Kuu msimu huu kutoka Ligi Daraja la kwanza hivyo zimejipanga kuleta ushindani katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

No comments: