Winga wa Yanga SC, Simon Msuva anatarajiwa kuondoka nchini kesho kuelekea nchini Morocco kwa ajili ya kukamilisha uhamisho wake kujiunga na Klabu ya Difaa Hassani El-Jadida ya Ligi Kuu ya nchini humo.
Msuva amesema, anaenda kucheza kimataifa ikiwa ni pamoja na kuendeleza kipaji chake pamoja na kujifunza soka la nje ya Tanzania na anaamini atapambana na changamoto atakazokutana nazo ili kusonga mbele zaidi ikiwa ni pamoja na kuwa na ushirikiano na winga Ramadhani Singano ‘Messi’ kutoka Azam FC ili kuweza kulitangaza zaidi soka la hapa nchini.
“Mungu akipenda safari ni kesho usiku na kingine nashukuru uongozi na mashabiki kwa sapoti waliyonionyesha, nitakwenda Morocco katika timu ya Difaa Hassani El-Jadida kumalizana nao kwasababu kila kitu kilikuwa tayari kwahiyo naenda kusaini pamoja na vipimo vya afya, walinipa ofa ya miaka minne lakini nimeafiki miaka mitatu ndiyo itakuwa mizuri zaidi" alisema Msuva
Mbali na hilo Msuva amewataka vijana ambao wanahitaji kusonga mbele katika soka kuwa na nidhamu nje na ndani ya kazi ili waweze kufanikiwa zaidi.
“Kikubwa mimi naamini ni nidhamu nje na ndani ya kazi unajua katika maisha ukiishi na watu vizuri chochote kinaenda sawa, kwahiyo nawasihi walio nyuma yangu wajitahidi tuu kwani chochote kinawezekana, kwasababu kama nimeonyesha mimi kutoka basi kuna wengine wanakuja na wapo wengine, nje na mimi naamini ndio wa kwanza Yanga hivyo naamini nyuma yangu kuna wengine wanakuja kama mimi” alisisitiza Msuva
Msuva amesema, Soka la nchini Morocco siyo mwisho kwake kwani matarajio yake ni kuweza kucheza La Liga.
“Ligi ya La Liga ndiyo ninayoifikiria sana, nikifika pale nitafanya vizuri zaidi ili nisogee pale na naamini hata miaka mitatu haitafika nitasogea zaidi" alisema Msuva
Msuva amesema, uwepo wa Winga Ramadhan Singano ambaye inasemekama yupo ndani ya Klabu hiyo itasaidia kuweza kulitangaza zaidi soka la Tanzania.
“Ushirikiano utakuwa mkubwa na itasaidia kwani ukiangalia kwa hapa Tanzania wapo Kamusoko na Ngoma wanatoka Zimbabwe na wana ushirikiano mzuri kwa hiyo tutashirikiana na kuangalia ni kitu gani kimetupeleka kule" alimalizia Simon Msuva
No comments:
Post a Comment