Serikali Kenya na Tanzania ziko mbioni kudhibiti ugonjwa wa Homa ya Chikungunya ambao huambukizwa na mbu aina ya aedes na hauna tiba mahsusi wala kinga.
Nchini Kenya, harakati bado zinaendelea kudhibiti mlipuko wa homa ya Chikungunya katika mji wa pwani wa Mombasa ambako hadi sasa watu 27 kati ya 154 waliofanyiwa uchunguzi wamethibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo.
Shirika la Afya duniani, WHO nchini humo linashirikiana na serikali kudhibiti mlipuko wa ugonjwa huo unaoenezwa na mbu ambao umekumba vitongoji vyote sita vya Mombasa ambavyo ni Mvita, Kisauni, Nyali, Changamwe, Jomvu na Likoni.
Nchini Tanzania Waziri wa Afya Ummy Ally Mwalimu ametoa tahadhari kwa umma kuhusu uwezekano wa kuenea homa hiyo ya Chikungunya baada ya kuibuka katika nchi jirani ya Kenya.
Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali na maumivu ya viungo, misuli, kichefuchefu na uchovu.
Ripoti za awali kabisa za kuwepo ugonjwa huo wa Chikungunya zilipatikana katikati ya mwezi uliopita ambapo kilichofuatia kilikuwa ni kukusanya sampuli za damu na kuziwasilisha kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi.
Ugonjwa wa Chikungunya unaweza kupunguzwa kwa kuchukua hatua kadhaa kukiwemo kuhakikisha mazingira ni masafi ili kuepusha mazalia ya mbu.
No comments:
Post a Comment